Waendesha bodaboda walaumiwa kwa ongekezo la visa vya dhulma za mapenzi kwa wasichana

kamishwa msaidizi wa eneo la Kisauni Benjamin Kipkorir amewanyoshea kidole cha lawama waendesha bodaboda akisema wamechangia sana kwa visa vya dhulma za mapenzi kwa wasichana ukanda wa Pwani.

Kipkorir amesema wasichana hao hudanganywa na pesa na kujipata kushiriki ngono na wanaume hao. Ameongeza kuwa wasichana hao hupata aibu kuripoti visa hivyo vya dhulma.

Afisa huyo amenena hayo kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa kulinda watoto hususan wasichana dhidi ya dhulma za kingono iliyoandaliwa na shirika la kimataifa la haki IJM pamoja na shirika la Global Fund.

Vilevile,Kipkorir ameeleza kuhuzunishwa na hali ya wasichana kuuza miili yao kwenye ufuo wa bahari ambapo baadhi yao huambukizwa magonjwa na kuacha shule.

Aidha amesema kuna uchache wa maeneo ya kuwapa hifadhi wasichana wanaodhulumiwa na zile zilizopo hazina rasilimali za kutosha.

Hafla hiyo vilevile imehudhuriwa na mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji ambaye amewatahadharisha wanaodhulumu wasichana kingono akisema afisi yake itahakikisha wameadhibiwa.

Shirika la IJM linanuia kulinda maelfu ya watoto kutoka familia maskini dhidi ya kuingizwa kwenye biashara za ngono, ukanda wa Pwani ukitajwa kuathirika pakubwa na uhalifu huo.