Naibu Gavana wa Taita Taveta awarai wanawake kujiingiza kwenye uongozi

Naibu gavana wa kaunti ya Taita Taveta Majala Mlagui (Picha Kwa Hisani)

Naibu gavana wa kaunti ya Taita Taveta Bi Majala Mlagui amehimiza wanawake kujiingiza katika uongozi na sekta  ya ajira akisema kuna nafasi kubwa ya wanawake kupata kazi.

Mlagui amenena hayo kwenye warsha iliyoleta pamoja wanawake katika rasilimali kazi ambapo wamejumuika kuangalia maswala yao katika utendakazi, kuzungumzia changamoto wanazopitia na kupata suluhu ya kufaulu katika utendakazi.

Kiongozi huyo ameeleza kutofurahishwa na asilimia ndogo ya wanawake katika nafasi za uongozi na sekta ya ajira.

Kulingana na takwimu,wanawake magava na naibu magavana ni asilimia 14, asilimia 22 wakiwa kwenye bunge la kitaifa na seneti na asilimia 23 wakiwa kwenye bodi za biashara.

Aidha,amedokeza ipo haja ya kuwapa wasichana na kina mama mwongozo ili kukomesha visa vya wasichana kupeana ngono ili kupata kazi.

Irene Kimacia kaimu mkurugenzi wa taasisi ya kimataifa ya rasilimali kazi IHRM naye amehimiza wanawake kuzingatia maadili mahali pa kazi.

Ameongeza kuwa  kasumba ya kwamba nafasi za siasa ni za wanaume ni potovu na wanawake wanaweza kujitegemea na kupenya katika siasa.