Maafisa wa usalama wanaoshirikiana na walanguzi wa dawa za kulevya kuchukuliwa hatua

Exif_JPEG_420

Imeandikwa na

 John Otieno

11/3/2021

Kamishna wa kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo amewatahadharisha maafisa wa usalama,machifu na wazee wa mitaa wanaoshirikiana na walanguzi wa dawa za kulevya akisema watachukuliwa hatua za kisheria.

Kitiyo amenena hayo Jumatano ya Machi 10,2021 Majaoni, alipozindua oparesheni ya kusaka walanguzi wa dawa za kulevya na wauzaji pombe haramu katika kaunti ya Mombasa, oparesheni hiyo ikitarajiwa kuchukua wiki mbili.

Kamishna huyo amedokeza suala la ulanguzi wa mihadarati limekuwa donda sugu kwenye kaunti hii,akieleza uhamasisho utafanywa kwa wananchi na maafisa wa usalama ili kusaidia katika vita dhidi ya mihadarati.

 

Ameongeza kuwa vijana watakaopatikana kwenye oparesheni hiyo watakabidhiwa shirika la kupambana na dawa za kulevya NACADA ili wasaidike na kupata sura mpya.

Mkurugenzi wa NACADA ukanda wa Pwani George Karisa ameeleza wasiwasi wake juu ya idadi kubwa ya vijana wanaotumia mihadarati kwenye kaunti ya Mombasa,takwimu zikionyeaha vijana 10,000 kutoka Mombasa wakiathirika,eneo la kisauni likiongoza.

“Kati ya vijana wa umri wa miaka 15-24 katika ukanda wa Pwani,asilimia 5.7 wanabugia pombe, asilimia 8.8 wanatumia sigara, asilimia 12.7 wanatumia miraa,asilimia 4.6 wanavuta bangi, asilimia 0.8 wakitumia heroin na asilimia 0.7 wakitumia kokein,”akasema Karisa.

Karisa amewataka wananchi kupiga ripoti kuhusu walanguzi na watumizi wa mihadarati kwa shirika la NACADA na asasi za usalama.

Vilevile, amedokeza serikali kuu na ya kaunti zinashirikiana kupeleka vijana kwenye vituo vya kujirekebisha licha ya changamoto za rasilimali zinazokabidhi vituo hivyo.

“Idadi ya vijana kwenye vituo vya kujirekebisha imekuwa kubwa kiasi cha kushinda idadi zinazotakiwa kubeba na rasilimali zilizopo kwenye vituo hivyo,” akasema Karisa.