Shirika la Lapaire Glasses lapeana huduma za matibabu ya macho bure

Shirika la Lapaire group kwa ushirikiano na shirika la Girls for Girls Africa pamoja na kampuni ya Diamond Trusties Limited walikongamana katika kituo cha watoto cha Wema Trust Foundation kupeana huduma za bure za macho,kuuza miwani kwa bei nafuu,kupeana ushauri wa kisaikolojia pamoja na kupeana mahitaji mengine muhimu  katika kituo hicho kwa watoto 105 cha Wema Trust Foundation.

Akiongea na wanahabari Afisa mkuu wa mawasiliano katika shirika la Lapaire Glasses,Oliver Wambile amesema wameamua kupeana huduma za macho bure na miwani kwa bei nafuu haswa baada ya kugundua watu wengi wanauhitaji wa huduma hizo lakini kutoka na ughali wa matibabu hayo wanasalia bila kutibiwa.

Kulingana na shirika la Afya nchini zaidi ya watu milioni 7 wana uhitaji wa huduma za macho ingawa wengi hawafanyiwi uchunguzi. Oliver amesema shiriko hilo ambalo lengo kuu ni kuhudumia watu wa bara la Afrika linapanga kuhudumia wananchi katika nchi zaidi ya 20 Afrika.

 

Kwa upande wake mwanzilishi wa shirika la Girls for Girls Afrika,Queentah Wambulwa amesema kuna haja kubwa ya wasichana kupata ushauri wa kisaikolojia haswa katika kipindi hiki cha Corona ambapo visa vya mimba za mapema pamoja na manyanyaso ya kijinsia yamekithiri.

Queentar amepongeza hatua ya kujengwa kwa vituo vya kusikiliza madhila wapitiayo wanawake ambapo wamekuwa mstari wa mbele kutatua matatizo hayo na hata kuhakikisha haki zao zinapatikana.

 

Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni ya Diamond Trust,Rafael Marende amesema kuna haja ya mashirika zaidi kujitokeza na kufanya miradi ambayo itasaidia jamii haswa katika kipindi hiki cha ujio wa Corona. Rafael amepongeza juhudi za Lapaire Glasses akisema ni za kupigiwa mfano.

 

Afisa wa mipango katika kituo cha watoto cha Wema Trust Foundation,Eunice Njoroge ameyashukuru mashirika hayo kwa ujio wao katika kituo hicho akisema huduma zao zimesaidia kituo hicho kwa kiwango kikubwa.

Eunice amewaomba wazazi kuwalea watoto wao katika misingi inayofaa ili kuwa mfano bora kwa vizazi vijavyo na pia kuepusha visa vya watoto kutoroka nyumbani na kurandaranda mitaani.