Usalama kuimarishwa Mombasa wakati wa msimu huu wa siku kuu

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa nchini Kenya Gilbert Kitiyo amewahakikisha wakaazi wa Mombasa kuwa usalama utaimarishwa wakati wa msimu huu wa krismasi.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kitiyo amesema kuwa polisi watashika doria maeneo yote ya Mombasa hususan maeneo bunge ya Nyali, Kisauni na Likoni.

Amewatahadharisha wanyakuzi wa ardhi, magenge ya uhalifu na kundi haramu la Mombasa Republican Council (MRC) akisema kuwa polisi wako macho na tayari kuzima visa vya uhalifu.

Kulingana na Kitiyo wanachama zaidi ya 60 wa kundi haramu la MRC walitiwa mbaroni na kuhukumiwa kifungo cha jela, mwezi mmoja uliopita, baadhi yao wakishindwa kulipia dhamana.

Kitiyo ameeleza kuwa wanafanya kazi kwa ukaribu na kaunti jirani zinazopakana na Mombasa kwa madhumuni ya kuimarisha usalama kwenye barabara kuu za kutoka nje ya kaunti hiyo ya Mombasa huku akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kuhusu ugaidi na uhalifu. Kaunti zinazopakana na Mombasa ni Kwale,Taita Taveta,Kilifi na Tana River.

Maeneo ya ikulu ya Mombasa, bustani ya Mama Ngina, Chuo cha matibabu KMTC, Huduma Centre, hospitali kuu ya mkoa wa Pwani, halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini KRA, kituo cha kitaifa cha utangazaji KBC, shirika la kukadiria ubora wa bidhaa KEBS na Mabenki kwenye kaunti ya Mombasa yatakuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Bahari na maeneo ya kuabudu zitatarajiwa kufuata kanuni zote za wizara ya afya za kujikinga dhidi ya virusi vya Corona,matatu zikitakwa kutobeba watu kupita kiasi.

Shamrashamra za kuwasha baruti ambazo hufanyika mkesha wa mwaka mpya hazitaruhusiwa kwani saa za kutotoka nje zitakuwa bado zinatekelezwa.

Kamishna huyo pia amewataka wananchi kujali afya yao wanaposherehekea siku kuu ya Krismasi wakati huu wa janga la corona ikizingatiwa kuwa Mombasa imerekodi idadi kubwa ya maambukizi ya corona watu 8,613 wakiathirika na 201 kuaga dunia tangu kisa cha kwanza cha corona kuripotiwa humu nchini.