“Hamtuwakilishi” KEMNAC yawaambia NAMLEF na CIPK

Viongozi wa KEMNAC na ALMADA katika hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano kati yao

Baraza la kutoa ushauri kwa waislamu nchini Kenya KEMNAC limepuzilia mbali madai ya mashirika ya NAMLEF na CIPK kama ilivyochapishwa kwenye gazeti moja nchini kuwa waislamu nchini wanapinga mchakato wa BBI wakisema kuwa hawakuhusishwa na kuwa hayo ni maoni yao pekee na wala si ya waislamu.

Baraza hilo limesema kuwa mashirika ya NAMLEF na CIPK yamekosa mwongozo katika jamii na kuwa ni vyama vya kisiasa vilivyojificha kwenye dini.

Kauli hiyo imejitokeza katika kikao na wanahabari ambapo KEMNAC pamoja na chama cha walimu wa madrasa nchini Kenya ALWADA wametia saini mkataba wa makubaliano utakaoleta mwongozo dhabiti na kuziba pengo la uongozi kwa waislamu nchini.

NAMLEF na CIPK zilipinga mchakato wa BBI zikisema kuwa pendekezo la kubuniwa kwa mahakama ya rufa ya waislamu haikujumuishwa kwenye ripoti ya BBI.

KEMNAC imesuta mashirika hayo ikisema hiyo si sababu tosha ya kupinga ripoti hiyo.Badala yake KEMNAC imesifia ripoti hiyo ikisema kuwa mapendekezo ya kubuniwa kwa mamlaka ya kusimamia mmea wa nazi,pamoja na suala la uchumi wa bahari ni faida kubwa kwa wapwani.

Baraza hilo limesema hatua ya pwani kuongezwa maeneo bunge, vijana kuwa na tume ya kushughulikia maswala yao pamoja na wawakilishi wadi kuwa na bajeti yao ni vigezo tosha vya kuunga mkono mchakato wa BBI.

Vilevile, KEMNAC imewapa makata ya siku kumi na nne NAMLEF na CIPK kutoa vyanzo vyao vya fedha watakazotumia kwenye kampeni ya kupinga mswada wa BBI kote nchini kama walivyosema huku wakiwasuta kwa kufeli kuwapa misaada maimamu na walimu wa madrasa wakati huu wa janga la corona.

“Misikiti na madrasa ilifungwa wakati wa corona.Maimamu na walimu wa madrasa wamepata shida hadi leo.Hamkuwapa chakula wala matibabu.Kuna maimamu na walimu wa madrasa walioambukizwa corona, hatukuona NAMLEF, CIPK wala mashirika yoyote,”akasema Juma Ngao mwenyekiti wa kitaifa wa KEMNAC.

Aidha,wameitaka serikali kuu kuruhusu mashirika yasiyokuwa ya serikali yaliyokuwa yakifadhili maimamu na walimu wa madrasa nchini kuendelea kutoa msaada huo wakiahidi kudhibiti mashirika hayo na pia kutambua madrasa kisheria na walimu wa madrasa wapate mishahara.