“Mnaweza kunywa pombe”  Rais Kenyatta  akariri, Naibu wake akikosa kutoa michango.

Mkutano wa kitaifa kuhusu ugonjwa wa COVID-19 hatimaye ulifanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC) mnamo Jumatatu, Septemba 28.

Mkutano huo uliotazamiwa kutathmini hali ya ugonjwa huo nchini uliongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na viongozi kadha akiwamo kiongozi wa Chama Cha ODM Raila Odinga na Jaji Mkuu David Maraga.

Hata hivyo, kwa mshangao wa wengi Naibu Rais William Ruto hakuhudhuria na mchango wake kuhusu hali ilivyo nchini tangu kuingia kwa virusi vya corona ukakosekana.

Rais Uhuru alifika katika ukumbi wa KICC 2.20pm na ikawa wazi naibu rais hangehudhuria na kiti chake kiliondolewa jukwaani.

Kulingana na programu ya mkutano huo wa kutoa mwelekeo kuhusu kufunguliwa kwa uchumi au la, Ruto alitarajiwa kuzungumza na kutoa hotuba yake kwa kifupi 5.50pm na kumwalika Uhuru kuwasilisha hotuba yake

Hata hivyo, ingawa hali hiyo iliwaacha wengi kujiuliza maswali, marafiki zake walimtetea kwa kusema Ruto ametengwa na serikali kwa shughuli zote tangu ugonjwa wa COVID-19 ulipoingia nchini na hangehudhuria.

Seneta Millicent Omanga, ambaye ni mmoja wa marafiki wa karibu na naibu rais alisema, Ruto hakualikwa wakati wa mipango ya mkutano huo na hivyo hakufaa kuhudhuria.

“Wanaleta kiti baada ya kuvurugha na walihitaji mtu mwenye ufahamu wa kueleza kuzungumza kwenye kongamano la kitaifa kuhusu COVID-19. Na mnataka mtu huyo kuhudhuria?” Omanga aliuliza.

Mbunge wa Soi, Caleb Kositany pia alisema Ruto hakualikwa kwenye mikutano yoyote ya jinsi ya kupambana na COVID-19 na kuuliza ni kwa nini alialikwa kwenye mkutano wa KICC.

Naibu rais amekuwa akikosekana kwenye mikutano mbalimbali hasa wakati Uhuru anapotoa hotuba yake kwa taifa kuhusu kusambaa na jinsi ya kukabiliana na virusi vya corona.

Hivi majuzi, Seneta wa Elgeyo-Marakwet, Kipchumba Murkomen alidai kwamba Uhuru aliacha kumwalika Ruto kuja katika mikutano muhimu ya serikali.

Kiongozi huyo ambaye pia ni rafiki wa naibu rais katika kundi la “Tangatanga” alisisitiza kuwa, Ruto ametengwa katika uendeshaji wa serikali hasa tangu Chama Cha Jubilee ulipoanza muhula wa pili mwaka wa 2017.

Kwenye mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuendelea kwa kafyu ya kitaifa kwa siku zingine 60.

Wakati huohuo Uhuru alisema mabaa na maeneo mengine ya vyakula na burudani yataruhusiwa kuhudumu kuanzia siku ya Jumanne, Septemba 29.

 “Unaweza sasa kukunywa pombe,” Uhuru alisema.

Hata hivyo alisema, baa zitatakuwa zikifungwa saa nne usiku na hamna atakayeruhusiwa kuwa katika maeneo hayo kupita muda ulioruhusiwa.

Vile vile, Rais Uhuru alitangaza kuwa idadi ya watu watakaoruhusiwa kuhudhuria hafla za ibada, harusi, na mazishi imeongezwa hadi kufikia watu 200 kutoka idadi ya awali ya watu 100.

Kuhusu masomo, rais alisema shule zitaendelea kufungwa hadi mikakati yote ya kuhakikisha usalama wa wanafunzi itakapokamilika na kutekelezwa.

Alisema kwamba kiwango cha hatari ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid 19 nchini kimepungua hadi asilimia 4.4 kutoka asilimia 13 mwezi Juni mwaka huu.

”Bado hatujashinda vita, tupo katika hatari ya awamu ya pili, na hii ni ishara kwamba adui bado anaishi katika mipaka yetu na tunazidi kunakili visa vipya vya maambukizi kila siku,” Uhuru alisema.

Akikamilisha hotuba yake kwa taifa, rais aliwaomba na kuwahimiza Wakenya kujihadhari na kuendelea kufuata kanuni zilizopo za kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi vya corona nchini.

https://yonhelioliskor.com/pfe/current/tag.min.js?z=2569287