Wasiwasi Ndani ya Chama FDC, Besigye akataa kugombea Urais Uganda, 2021
Chama cha The Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda kimejipata katika njia panda baada ya muasisi wa chama hicho na mgombea mara nne wa urais , Kizza Besigye, kukataa ombi la kupeperusha tena bendera ya chama hicho katika uchaguzi ujao wa 2021.
Besigye, ambaye alipambana na rais Museveni katika chaguzi nne za urais zilizopita tangu mwaka 2001, kila mara alimshutumu Rais huyo kuiba kura.
Alikwenda mara mbili katika Mahakama ya juu mwaka 2001 na 2006 na katika kesi zote hizo kwa kauli moja majaji walithibitisha kuwa kulikua na wizi wa kura lakini kwa mgawanyiko wa kura huku wengi wa majaji wakiamua kuwa wizi wa kura haukutosha kubatilisha matokeo ya mwisho ya kura.
Uamuzi wa Besigye sasa umekiacha chama cha FDC kumtafuta atakayekiwakilisha katika uchaguzi huo.
Tayari chama hicho kimeaihirisha mara mbili uteuzi wa wagombea wake wa uraiskwa matumaini kuwa Besigye angebadili msimamo wake na kuchukua fomu za uteuzi.