Maelfu wapoteza makaazi Oromia Ethiopia
Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema zaidi ya watu elfu 9 wamepoteza makazi yao kutokana na vurugu zilizotokea katika jimbo la Oromia katikati ya Ethiopia.
Ripoti iliyotolewa na OCHA imesema maandamano pia yameathiri operesheni za kibinadamu, ugawaji wa chakula na operesheni nyingine muhimu, ikiwa ni pamoja na operesheni za kupambana na virusi vya Corona. Ripoti hiyo pia imesema vurugu katika jimbo la Oromia zimepunguza upimaji wa virusi vya Corona na kukwamisha ufuatiliaji wa watu wanaodhaniwa kuambukizwa virusi vya Corona.
Mwezi uliopita maandamano ambayo wakati mwingine yalibadilika kuwa vurugu mjini Addis Ababa na kwenye miji mengine katika jimbo la Oromia yalitokea baada ya mwanamuziki maarufu wa kabila la Oromia Huchalu Hundessa kuuawa na watu wasiojulikana. Baadaye serikali ilisema watu 239 waliuawa na wengine karibu elfu 10 walikamatwa kwenye vurugu.