Seneta Miraj Abdillahi aunga mkono mpango wa wafanyikazi kuchangia ujenzi wa nyumba za bei nafuu

SENETA maalum wa kaunti ya Mombasa kupitia chama cha UDA Miraj Abdillahi ameutetea mpango wa serikali ya kitaifa wa kuwataka wafanyikazi kuchangia asilimia tatu ya mishahara yao ili kufadhili ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Akihutubia katika hafla ya kuzinduliwa kwa vuguvuvu la sauti ya Mombasa ambalo linatarajiwa kuleta mwamko wa mpya wa  kisiasa na kiuchumi kwenye kaunti ya Mombasa , Miraj ameupongeza mpango huo wa serikali ya kitaifa, akisema kuwa unalenga  kuhakikisha kila mkenya anamiliki makaazi nadhifu na kwa bei nafuu.

Kulingana na Miraj mpango huo endapo utatekekezwa kikamilifu  utaiepusha serikali dhidi ya kuchukuwa mikopo yenye riba ya juu kutoka ya mataifa nje ili kufadhili ujenzi wa nyumba hizo  sawia na  kudhibiti  kwa kiasi kikubwa mikopo ya kiholela inayochukuliwa na serikali ya kitaifa kwa ajili ya kufadhili miradi ya maendeleo nchini.

Wakati huo huo Miraj amemrai waziri wa uchukuzi nchini Kipchumba Murkomen kuidhinisha  mara moja ndege zote za kimataifa kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi jijini Mombasa ili kupiga jeki shughuli za utalii na uwekezaji kwenye kaunti ya Mombasa na eneo la pwani kwa ujumla.

Mbali na hayo miraji amedokeza kuwa ndani ya kipindi cha wiki mbili zijazo watamjarajia  rais William Ruto kuhudhuria kwenye hafla kutolewa kwa hati miliki za ardhi ya Bububu kwa wakaazi eneo hilo baada ya kutatatuliwa kwa utata uliyoshuhudiwa awali kuhusiana na umiliki wa kipande hicho cha ardhi.