Hatimaye Ruto kuapishwa jumanne ijayo

Kamati ya mpito iliyotwikwa jukumu la kusimamia upokezaji  wa mamlaka imetangaza jumanne kuwa  siku ya likizo kwa ajili ya Kumuapisha rais mteule William Samoei  Ruto pamoja na naibu wake Rigathi Gachagua.

Kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo Joseph Kinyua amebainisha kuwa hafla ya kumuapisha rais Mteule pamoja na naibu wake itaandaliwa katika uga wa kasarani jijini Nairobi mnamo tarehe kumi na tatu mwezi huu kati ya saa nne asubuhi na saa nane mchana kama inavyohitajika kisheria.

Hatahivyo akiongea katika kikao na wanahabari katika jumba la Harambee jijini Nairobi Kinyua amesema kuwa tangazo kuhusu likizo ya siku  hiyo litachapishwa katika gazeti rasmi la serikali baadaye wiki hii huku akiongezea kuwa zoezi hilo zima  litafwatwa kama lilivyoanishwa katika katiba

Kulingana na katiba rais mteule anapaswa  kulishwa kiapo na msajili mkuu wa mahakama mbele ya jaji mkuu .

kikao hicho cha  leo kinajiri siku moja tu baada ya mahakama ya upeo nchini kumuidhinisha rasmi William Ruto kuwa rais mteule  baada ya uamuzi wa majaji saba hapo jana  kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa katika mahakama hiyo  kupinga  kuchaguliwa kwake kama  rais wa tano wa taifa hili..