SHAHBAL APINGA KURA ZA MAONI, ASHINIKIZA WAPINZANI KUPAMBANA KWENYE MCHUJO

Mgombea Ugavana wa ODM Mombasa

Huku zoezi la kura za mchujo za chama cha ODM likikaribia, joto la kisiasa linaendelea kushamiri kaunti ya Mombasa na viongozi wakiendelea kurushiana cheche za lawama kufuatia ripoti ya kura za maoni iliyotolewa hivi majuzi.

Kutokana na ripoti kuibuka kuwa chama cha ODM kimepania kutoandaa kura za mchujo kaunti ya Mombasa na badala yake kutoa tiketi kwa mgombea mwenye umaarufu kupitia kura za maoni.

Hatua hiyo imezua gumzo huku viongozi wamepinga vikali na kukishinikiza Chama cha ODM kusimamia demokrasia kwa kuandaa kura za mchujo zitakazokuwa huru na haki kwa wagombea wote kaunti ya Mombasa.

Katika kikao na zaidi ya wagombea 150 wa nyadhfa mbalimbali wa chama hicho kaunti ya Mombasa, mgombea Ugavana Suleiman Shahbal amepinga suala la kutolewa kwa tiketi ya moja kwa moja kwa wagombea kwa kigezo cha umaarufu au kura za maoni.

 

Mgombea Ugavana Mombasa kwa tiketi ya ODM. Picha kwa Hisani

Vilevile Shahbal amepuuzilia mbali kura za maoni zilizotolewa na mashirika mbalimbali zikionesha umaarufu wa mpinzani wake mkuu kuwa juu, huku  akisisisitiza kuandaliwa kwa kura za mchujo badala ya kutoa tiketi kwa njia ya moja kwa moja.

Wakati huo huo Shahbal ametahadharisha uongozi wa chama cha ODM dhidi ya kuingilia demokrasia na haki ya wakazi wa Mombasa kwa kuwachagulia viongozi, akisema kuwa hatua hiyo inayoendelezwa katika sehemu mbalimbali nchini huenda ikaathiri umaarufu wa chama hicho katika kaunti hii.

Haya yanajiri siku kadhaa baada ya tetesi kuibuka kuwa ODM imepanga kupeana tiketi ya moja kwa moja kwa mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharif Nassir kutokana na umaarufu wake kuwa mkubwa baada ya kura a maoni kumuweka kileleni dhidi ya wagombea wengine.

Hata hivyo chama cha ODM kilitangaza kuahirisha zoezi la kura za mchujo kaunti za Mombasa na Kilifi lililokuwa limepangwa kufanyika kati ya tarehe 6 na 7 mwezi huu, ili kufanya mazungumzo kabla ya kutoa mwelekeo wake.

 

 

 

https://itweepinbelltor.com/pfe/current/tag.min.js?z=2569287