Viongozi wa kidini wataka wanasiasa kukoma kutoa matamshi ya chuki

Wanachama wa CICC kwenye mojawapo ya warsha zao Picha kwa hisani

Muungano wa viongozi wa kidini ukanda wa Pwani nchini Kenya CICC umetoa wito kwa wanasiasa kukoma kutoa matamshi ya chuki yatakayosambaratisha nchi hii na hata kuleta ghasia haswa wakati huu ambapo siasa zimepamba moto nchini.

CICC imewataka viongozi hao kutotumia upungufu ulioko kwenye jamii na kupanda maneno ya chuki miongoni mwa watu na badala yake kutumia uhuru wa kujieleza vizuri wakisema kuwa nchi hii ni kubwa kuliko mtu yeyote na lazima kuwe mazingira mazuri kwa wote.

“Tunatoa wito kwa wanasiasa kukoma kuchochea wakenya ambao watarudi kwao baadaye kuomba kura.Tunawahimiza viongozi wote licha ya nyadhifa zao kuheshimiana na kutotoa matamshi ya chuki yatakayochangia ukosefu wa amani na hatimaye vifo na mali kuharibika,” alisema Sheikh Sharif Mandhar mwenyekiti wa baraza la waislamu nchini Kenya SUPKEM.

Kauli yao inajiri siku chache baada ya ghasia na vuta nkuvute kushuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Msambweni ambapo wanasiasa waliokuwa wakimuunga mkono mgombea huru Feisal Bader kuonekana kuvurutana na wanasiasa waliokuwa wakimuunga mkono mgombea kupitia chama cha ODM Omar Boga wananchi taswira iliyoleta picha mbovu kwa wakaazi wa Msambweni.

Viongozi hao wametaka tume ya utangamano na maridhiano nchini NCIC na Idara ya Upelelezi wa Jinai DCI kuchukulia hatua wanasiasa na viongozi watakaopatikana wakitoa matamshi ya chuki wakiwataka viongozi wa dini kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa amani.

Aidha,CICC imeitaka serikali kuu kusuluhisha migogoro ya madaktari kwani wakenya wanategemea pakubwa hospitali za serikali hususan wakati huu wa janga la corona.