Je,ukosefu wa maadili unachangia uaviaji wa mimba miongoni mwa wasichana wadogo?

Suala la uaviaji mimba miongoni mwa wasichana, linazidi
kusheheni katika Kaunti ya Mombasa hususan wakati huu wa
janga la corona,wasichana walio na umri wa chini ya miaka 18
wakiangukia mtegoni na kuathirika zaidi.

Hali hii imezua mjadala si mitandaoni pekee bali vitongojini
hadi majumbani mwetu.Maswali yanazidi kuibuka, nani
wakulaumiwa?

Fatuma (si jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 15,
alilazimika kuavya mimba baada ya mpenziwe kukata kuchukua
majukumu.

Anakiri kukosa mwelekeo baada ya kupokea taarifa hizo kutoka
kwa mpenziwe, ikizingatiwa kuwa kwao ni maskini, akilelewa
na mamake pekee na hakuwa na namna ya kumlea mtoto huyo
endapo angejifungua.

Vitendo vya kuavya mimba ndivyo vinayomsikitisha Bi
Corazon Amukhala,mkurugenzi katika shirika la kutetea haki za
watoto hususan wa kike la Decent Conversation Foundation,
lenye afisi zake kwenye kitongoji duni cha Jomvu katika Kaunti
ya Mombasa.

Bi Amukhala anasema kuwa changamoto wanazopitia
wasichana kama Fatuma wakiwa wajawazito ndizo huwasukuma
kuavya mimba.

Mkurugenzi huyo anasema kuwa wasichana hao hulelewa katika
mazingira ya umaskini na huingia uoga wakati aliyewatunga
mimba hukata majukumu.

Amukhala anakiri kukumbwana changamoto kushawishi
wasichana hao kulea ujauzito kwani wenzao wa rika
huwashawishi kuavya mimba ikizingatiwa mazingira
wanayokuwemo.

Vilevile, anaelekeza kuwa ukosefu wa sodo kwa wasichana
wadogo huwasukuma kwenye mahusiano ili kupata bidhaa hiyo
muhimu kwao.

Kwa mujibu wa takwimu ya mwaka 2012, iliyotolewa na
Shirika linaloshughulikia afya ya baada ya uaviaji mimba humu
nchini POST ABORTION CARE (PAC), inaonyesha kuwa
asilimia 78 ya wanafunzi katika taasisi zote za masomo
waliripotiwa kuavya mimba.

Ikizingatiwa wakati huu wa janga la corona, idadi hiyo
inakadiriwa kuongezeka kutokana na wanafunzi wengi kusalia
manyumbani baada ya shule kufungwa mwezi machi mwaka
huu 2020.

Sheikh Mohamed Khalifa katibu katika baraza la wahubiri na
maimamu nchini Kenya analalama kuwa maadili ya malezi ya
kidini na jamii yamekosa nafasi katika kizazi cha sasa hivyo basi
kuchangia ongezeko la visa vya uaviaji mimba miongoni mwa
wasichana wadogo.

Khalif anasema kuwa kizazi cha sasa kinafwata mambo ya
wazungu, watoto wakiwepa uhuru kupita kiasi na wazazi
wanapowaadhibu watoto wao, wanakemewa baadhi yao
wakishtakiwa kwenye vituo vya polisi.Ameilaumu vyombo vya
habari kwa kuonyesha video chafu.

Kiongozi huyo wa kidini ameeleza kuwa watoto hao
wanapopata mimba hukosa mwelekeo hivyo basi kuavya mimba
bila kujali matokeo na madhara yake.

Amewataka wasichana wadogo kuwa makini ili wasinyanyaswe
na kujiepusha na tamaa ya kutaka kuwa na simu wakiwa bado
wachanga na kutovaa nguo za kubana.

Vilevile, Khalif ametaka jamii ikumbatie mila na desturi za
zamani ili kuzuia visa vya kuavya mimba kutoripotiwa.

“Watu warudi katika mila zetu. Wavae nguo za
heshima.Runinga zidhibitiwe.Wazazi wasiingiliwe
wanapowaadhibu watoto wao,” alisema Sheikh Mohamed
Khalif.

Mwandishi; Jane Meza Mwanza