Ushirikiano miongoni mwa wananchi ndio suluhu ya kupambana na ufisadi asema Guchu

Katibu mwandamizi katika afisi ya mwanasheria Mkuu na Idara ya Haki Winnie Guchu Picha Kwa Hisani

Katibu mwandamizi katika afisi ya mwanasheria mkuu na idara ya haki nchini Kenya Winnie Guchu ameeleza matumaini yake kuwa vita dhidi ya ufisadi nchini humo vitafaulu iwapo kutakuwa na ushirikiano miongoni mwa wananchi.

Bi Guchu amesema hayo baada ya kukutana na mwakilishi wa kamishna wa Kaunti ya Mombasa na kamati ya uangalizi ya kaunti hiyo ya kupambana dhidi ya ufisadi CCOC ambapo ametathmini utendakazi wa kamati hiyo na kujadili jinsi wanavyoweza kusaidia kamati hiyo katika utendakazi wake.

Katibu huyo amesisitiza kuhusu uhamasishaji wa umma kuhusu madhara ya ufisadi huku akiwataka kuripoti visa vyote vya ufisadi kama miradi iliyosimama na uwizi wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa miradi hiyo hususan kwenye miradi ya serikali kuu na ile ya kaunti.

Kamati ya CCOC inajumuisha wawakilishi kutoka kila kaunti ndogo za Mombasa, majukumu yao yakiwa kuhamasisha jamii kuhusu vita dhidi ya ufisadi, kukagua na kuhakikisha kuwa miradi ya serikali kuu pamoja na zile za serikali za kaunti na hazina ya maeneo bunge CDF zimekamilika baada ya kuhamasisha wananchi kuhusu miradi katika maeneo bunge yao, kiasi cha fedha kilichotengewa miradi hiyo, kampuni zilizokabindhiwa kandarasi hizo na asasi zipi zinazosimamia miradi hiyo.

Mwenyekiti wa CCOC Asha Mulo amesema wanapata ugumu wanapoulizia taarifa kuhusu miradi inayoendelea hata baadhi maafisa wao, wakikamatwa.

Vilevile, baadhi ya Wananchi huogopa kuwapa taarifa wanazozihitaji wakihofia usalama wao. Wakati mwingine kamati hiyo hupokea taarifa za uongo hali inayodidimiza utendakazi wao.