Kenya yaadhimisha siku ya UKIMWI duniani

Zaidi ya asilimia 96 ya watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI nchini Kenya wako kwenye matibabu huku asilimia 90 ya idadi hiyo wakidhibiti makali ya virusi vya HIV hivyo basi kupunguza uwezekano wa kusambaza virusi hivyo.

Akizungumza katika hafla ya kutoa ripoti kuhusu maambukizi ya virusi vya corona nchini Kenya, Katibu Mwandamizi katika wizara ya Afya Rashid Aman amesema kuwa taifa hilo limeshuhudia upungufu wa maambukizi mapya ya HIV.

Mwaka 2012 watu 106,000 waliripotiwa kuambukizwa HIV, idadi hiyo ikapungua kwa watu 36,000 mwaka 2018, hatua inayoonyesha Kenya imesonga mbele katika kudhibiti janga hilo.

Watu milioni 1.1 wamenufaika na dawa za kupunguza makali ya virusi vya HIV, katibu Aman akitaja ushirikiano kati yao na wadau, mashirika pamoja na uongozi dhabiti ndio imechangia maendeleo hayo.

Aman ametaja janga la Corona kuwa changamoto katika shughuli ya kupima watu maambukizi ya virusi vya HIV kwani watu wachache hujitokeza wakati huu wa janga hilo.

Idadi ya watu wanaojitokeza kujua hali yao ya HIV imepungua kati ya Januari , 2019 na Juni, 2020 viwango hivyo vikipungua kwa asilimia 33 mwezi wa Machi na Aprili mwaka huu 2020.

Vilevile, kulikuwa na upungufu wa watu wanaojisajili kupokea dawa za kupunguza makali ya virusi vya HIV kati ya Januari, 2018 na Julai, 2019 upungufu huo ukiendelea kushuhudiwa hadi Juni, 2020.

Wakenya wamehimizwa kutafuta huduma za afya , wakati ambao Kenya imerekodi visa 551 vipya vya maambukizi kati ya sampuli 4,675 zilizopimwa Jumanne ya Desemba 1, 2020. Watu 5 wameaga dunia.

Wagonjwa 266 wamepata nafuu, 206 kati yao walikuwa wakitibiwa nyumbani huku 60 wakiruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitali tofauti nchini Kenya.

Watu 1,275 bado wamelazwa hospitalini wakiugua Virusi vya corona, 8,070 wanatibiwa wakiwa nyumbani. Wagonjwa 71 wako katika chumba cha watu wenye hali mahututi,36 kati yao wakitumia ventileta na 34 wanatumia mitungi ya kupumua hewa safi.