Wito kwa Jamii kutambua Uwezo wa Vijana na Kuwaendeleza

Mkurugenzi wa Halmashauri ya maendeleo Pwani CDA Beatrice Gambo amepongeza juhudi za Vijana wanaojizatiti kujikimu kimaisha kwa kukumbatia ajira binafsi.

Akiongea katika hafla ya kuhitimu kwa wanafunzi wa chuo cha Uokaji cha Minat, Bi. Gambo amemtambua mwanadada Amina Khalid binti wa miaka 21 kwa juhudi zake katika kujiendeleza na hata kumiliki kampuni ya Minat bakery, akimtaja kama mfano wa kuigwa na vijana.

Bi. Gambo aliyemwakilisha mfadhili wa hafla hiyo Suleiman Shahbal ameapa kushirikiana na Minat  ili kumwezesha kuwafunza vijana wengi zaidi taaluma hiyo ya uokaji.

Huku hayo yakijiri Gambo amesema tayari vijana zaidi ya 50 kutoka eneo la Buxton wanafaidika na mafunzo katika chuo cha kiufundi cha NITA kupitia mradi wao wa ujenzi wa nyumba za kisasa unaotarajiwa kufanyika katika eneo hilo.

Aidha mafunzo hayo yanapania kuwafaidi vijana pindi mradi huo utakapoanza na pia kujiweka katika nafasi za kupata ajira katika miradi mbalimbali kama vile Dongo Kundu.

Vile vile ameonfgeza kuwa wamepanga kuwajumuisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za kaunti ya Mombasa katika miradi mingine.

Gambo amewarai wazazi kuwaunga mkono watoto wao na kuwasaidia katika kukuza talanta zao.