NEPAD na APRM yazindua ripoti kuhusu uongozi nchini Kenya

(Kutoka Kushoto) Kamishna wa kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo,katibu mwandamizi katika wizara ya fedha na mipango Nelson Gaichuhie na Mkurugenzi wa NEPAD/APRM Elias Mbau

Shirika la NEPAD kwa ushirikiano na The African Peer Review Mechanism (APRM) chini ya Muungano wa Afrika (AU) imezindua ripoti ya pili kuhusu uongozi nchini Kenya.

Katika Ripoti ya pili iliyozinduliwa na mashirika hayo, Kenya imepiga hatua katika uongozi kwa kuongeza viwango vya demokrasia nchini,kuimarisha uhuru wa idara ya mahakama, kuleta ugatuzi nchini, kuzindua katiba mpya,uwepo wa ofisi za huduma yaani Huduma centers miongoni mwa masuala mengine.

Kando na Demokrasia, siasa,uongozi na usimamizi wa uchumi ripoti hiyo imetaja ufisadi, kukosekana kwa uongozi bora hususan kwenye nyadhifa za kazi.

Aidha , ripoti hiyo imependekeza kuboreshwa kwa ushiriano kati ya asasi za usalama , wananchi kujumuishwa kikamilifu katika uongozi ,kuunda mazingira bora kwa wafanyabiashara wadogowadogo vijijini kufanya biashara zao,kushirikiana na kudumisha mahusiano na washikadau kama njia zitakazosaidia nchi.

Akizungumza na vyombo vya habari kaunti ya Mombasa Mkurungenzi wa Mashirika ya NEPAD na APRM Elias Mbau ametaka serikali za Kaunti kukubali ombi lao la kutaka serikali za kaunti kukaguliwa kuhusu masuala ya uongozi ili kubaini utendakazi wao pamoja na kuboresha uchumi wa kaunti.

Kwa upande wake Katibu Mwandamizi katika wizara ya fedha na mipango Nelson Gaichuhie amesema kuwa mpango wa kushirikisha serikali za kaunti ni njia ya kaunti kuweza kujisimamia.

Gaichuhie amepongeza mapendekezo kwenye BBI ya kupatia kaunti asilimia 35 ya fedha za bajeti akisema ukaguzi wa utendakazi kwenye kaunti utasaidia wizara ya fedha kujua namna fedha hizo zimetumika kwenye kaunti.

“BBI inataka kuleta pesa nyingi kwenye kaunti, kama wizara ya Fedha tutakuwa na furaha kama fedha hizo ( Asilimia 35 ya bajeti kwa kaunti) zitatathminiwa na kujua zimefanyia nini mwananchi,”akasema Gaichuhie.

Shughuli hiyo inanuia kuboresha viwango vya uongozi barani Afrika na kuainisha malengo ya nchi hizo kuhusu maendeleo iwe sawa na ya Muungano wa Afrika, AU.

Kenya ilikuwa nchi ya tatu barani Afrika kukubali kukaguliwa na APRM mwaka wa 2006 miaka mitatu baada ya kusaini makubaliano ya kuruhusu kukaguliwa.