Maelekezo mapya yatolewa na baraza la viongozi wa dini nchini

Baraza la viongozi wa dini nchini Kenya imetoa mwongozo mpya wa kuzingatiwa katika maeneo ya dini nchini wakisema kuongezeka kwa idadi ya visa vya maambukizi ya corona na vifo vya corona zimewafanya kufikia uamuzi huo.

Kasisi Connie Kivuti ,Naibu mwenyekiti wa baraza hilo amesema muda wa ibada utakuwa dakika tisini, watu 50 pekee ndio watakaoruhusiwa kwenye harusi , huku familia za kinasaba pekee zikiruhusiwa kula harusini.

Watu 100 ndio wanaoruhusiwa kwenye matanga , 15 wakikubaliwa kuwa kaburini wakati wa mazishi. Hakuna chakula kitakacholiwa mazishini. Ibada ya mazishi itachukua saa moja.

“Tunataka viongozi wa dini kufanya kazi kwa karibu na serikali kuu na asasi za usalama kwenye magatuzi zao ili kuhakikisha sheria hizi za matanga zimezingatiwa,” alisema Kasisi Kivuti.

Vilevile, hakuna mikutano itakayofanyika kwenye maeneo ya dini.

Baraza hilo limesema maombi ya watu binafsi kwenye maeneo ya dini itaanza Ijumaa,Novemba 27,2020.

Aidha , baraza hilo limetoa wito kwa serikali kufanya mazungumzo na wahudumu wa afya na kusuluhisha matatizo yanayokumba sekta ya afya ili wakenya wapate huduma bora za afya wakati huu wa janga la corona.