Mabaharia wa Kenya wataka ripoti ya fedha kutolewa

Picha kwa hisani

Wanachama wa chama cha mabaharia nchini Kenya (SUK) wameutaka uongozi wa chama hicho kutoa ripoti za matumizi ya fedha ya chama hicho kabla ya msajili wa vyama vya wafanyakazi kusimamisha shughuli za chama hicho.

Katika mahojiano ya kipekee, mmoja wa wanachama wa chama hicho SUK Albert Adembesa, amewashtumu viongozi wakuu wa chama cha Mabaharia nchini humo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Adembesa alisema kwamba, viongozi hao wamefeli kutuma ripoti za fedha za chama tangu 2016 hadi mwaka huu 2020 kwa msajili wa vyama vya wafanyakazi nchini Kenya huku Adembesa akisema kuwa takriban Shillingi milioni 10 zikiripotiwa kufujwa na viongozi hao.

“Tulikuwa tunataka tuambiwe makadirio ya fedha na vipi hizi fedha zimetumika bila wanachama kuarifiwa na kwa sababu gani hakukuwa na mkutano wa mwaka,”alisema Adembesa.

Ukaidi huo unatishia kuyumbisha nguvu za chama hicho ambacho kinategemewa pakubwa na mabaharia wanachama.

kamishna wa Polisi katika Kaunti ya Mombasa hakuidhinisha mkutano wao ulionuiwa kufanyika jana, Alhamisi ya Novemba 19, 2020 huku wanachama hao wakimlaumu Katibu Mkuu wa chama hicho Stephine Owaki kwa kuhujumu juhudi zao za kutaka uwajibikaji.

“Tunasikitika na hatua ya kamishna wa Polisi kuukata huu mkutano. Ni kitu kinatuumiza .Tunataka serikali iingilie kati kwa undani kwa kuwa sisi tunachouliza ni pesa zetu,” alisema Kassim Nguta ambaye pia ni mwanachama wa chama cha Mabaharia.

Mkutano huo ulinuia kupokea ripoti kuhusu matumizi ya fedha na makadirio ya bajeti ya chama hicho na kuchagua viongozi watakaosimamia uchaguzi wa chama hicho mwaka ujao 2021 kwa mujibu wa katiba ya chama chao.

Hii itakuwa ni mara ya pili chama hicho kusimamishwa, endapo msajili wa vyama vya wafanyakazi atafanya hivyo.

Wakuu wa chama hicho walijiuzulu wakiwemo mwenyekiti Daudi Hajji, naibu katibu mkuu Saidi Chako, mwekahazina Babu Mwinyi Babu pamoja na naibu wake Zelda Nzigha huku Katibu Mkuu Stephine Owaki akibakia afisini.

Aidha, wanachama hao wamemkashifu Katibu wa kudumu anayesimamia idara ya ubaharia kwenye wizara ya uchukuzi Nancy Karigithu wakisema kuwa anahujumu haki za mabaharia na kuingilia maswala ya chama chao.

Wametaka waziri wa leba Simon Chelugui kuingilia kati na kutatua swala hilo , wakiapa kuwapeleka kortini viongozi hao endapo hawatotimiza matakwa yao.