Gideon Moi arai vijana kuunga mkono BBI

Seneta wa Kaunti ya Baringo Gideon Moi Picha kwa hisani

Seneta wa kaunti ya Baringo nchini Kenya Gideon Moi amewarai vijana kuunga mkono ripoti ya jopo la upatanishi BBI.

Amesema ripoti hiyo itawezesha vijana kupata takribani asilimia thelathini ya mgao wa fedha kwenye kaunti wanazoweza kutumia kujiendeleza na kufanya biashara.

Moi, ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha KANU, amesifia ripoti hiyo akisema itawaunganisha wakenya na kuwarai wajisome ripoti yenyewe.

Seneta huyo ameeleza matumaini yake kuwa maswala ibuka ya wafugaji yatajumuishwa kwenye ripoti ya mwisho ya BBI.

Moi amekuwa katika kaunti ya Kajiado Jumanne ya Novemba 17, 2020 akikagua miradi ya maendeleo pamoja na gavana wa kaunti hiyo ya Kajiado, Joseph Ole Lenku huku wakizindua kituo cha kuhifadhi damu.

Kauli yake inajiri wakati ambapo taifa la Kenya likiwa limegawanyika kati ya wale wanaoikubali ripoti ya BBI jinsi ilivyo au wale wanaoitaka ifanyiwe marekebisho.

Shughuli ya kukusanya sahihi za kura ya maamuzi itazinduliwa Alhamisi hii ya November 19, 2020 na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga.