Wasafiri na Wahudumu wa matatu Roho mkononi kwa kukiuka sheria za COVID-19 – Mombasa

Kulingana na afisa mkuu wa polisi eneo la Changamwe  Mjini Mombasa, Joseph Kavoo, zaidi ya magari mia moja ya usafiri yalinaswa wakati wa msako uliofanywa na maafisa wa trafiki mapema Oktoba 28.

Kavoo alisema watu wote waliokamatwa walipelekwa katika kituo cha polisi cha Changamwe na watafikishwa mahakamani kabla ya siku ya Jumanne, Oktoba 27 kuisha

Akizungumza na wanahabari, Kavoo alisema wasafiri hawakuwa wamevalia barakoa, wahudumu wa matatu nao hawakuwa wameweka maji na sabuni au sanitaiza kwenye magari yao.

Kavoo alisema washukiwa watashtakiwa kwa kuvunja sheria zilizowekwa na wizara ya afya za kuzuia maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Kulingana na sheria hizo, “ Mtu yeyote ambaye atapatikana akikaidi sheria za COVID-19, atapigwa faini ya KSh 20,000 au kifungo cha miezi sita gerezani au atahukumiwa zote mbili.”

Viongozi kaunti ya Mombasa wamekuwa wakilalama kuhusu ongezeko la maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Akiwahutubia wakazi siku ya kuadhimisha sherehe za Mashujaa, Gavana wa Mombasa Hassan Joho aliwasihi wazingatie masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.Joho alisema huenda kaunti hiyo ikafungwa tena endapo wakazi wataendelea kuchukulia ugonjwa huo kwa mzaha.