Chama cha wauguzi tawi la Mombasa latishia kuitisha mgomo

 

Chama cha wauguzi (KNUN) tawi la Mombasa limetishia kuitisha mgomo wiki ijayo iwapo serikali ya kaunti ya Mombasa haitotilia maanani matakwa yao.

Kupitia katibu wao Peter Maroka , chama hicho kimetaja kutolipwa mishahara yao kwa wakati kuwa miongoni mwa sababu ya wao kuafikia uamuzi huo.

Peter amedokeza kuwa wauguzi hao hawajalipwa mishahara ya mwezi wa oktoba na ni hapo jana ndipo mishahara ya mwezi wa Septemba ya baadhi ya wauguzi ililipwa licha ya kuwa walihitaji fedha hizo kutosheleza mahitaji yao.

Kiongozi huyo amesema wauguzi hawana vifaa mwafaka vya kuwahudumia wagonjwa wa korona na kuchangia kuongezeka kwa maambukizi miongoni mwa wauguzi akitaja kuwa wauguzi sita wameambukizwa virusi vya korona wiki mbili zilizopita na wawili kupoteza maisha yao.

Ameisuta serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kile alichokitaja kama kutochukulia kwa uzito swala la madaktari.

Chama hicho vilevile kimetaka tume ya kuratibu mishahara (SRC) na serikali ya kaunti ya Mombasa irudishe marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira hatari.

Chama hicho kimetaka wenzao wa diploma ya juu kupandishwa vyeo na kuiomba wizara ya leba kuchapisha ugonjwa wa korona katika gazeti la serikali kama ugonjwa unaoathiri ajira zote.