Ajabu ya sheria: Korti yamzawidi aliyekuwa katibu wa Serikali shilingi moja Kama fidia.

Mahakama imesema aliyekuwa katibu katika wizara ya Ugatuzi, Lillian Omollo kulipwa shilingi moja kwa kuachishwa kazi kwa njia isiyofaa.

Mahakama ya kutatua migogoro ya waajiri na waajiriwa nchini, imeamua Oktoba 22 kuwa Omollo hakupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kuachishwa kazi.

Jaji Stephen Radido alisema haki za Omollo kikatiba kama mwajiriwa katika afisi ya rais zilikiukwa.

Alisema alifaa kupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kutimuliwa kwa hivyo akaagiza alipwe shilingi moja.

Mlalamikaji hakupewa nafasi ya kujibu, wala hakupewa sababu za kuondolewa kwa afisi chini ya mkono wa Rais. Alijulishwa kuwa kazi ilikuwa imeisha kwa sababu mtu mwingine alikuwa ameteuliwa kuchukua wadhifa huo,” alisema.

Mlalamikaji anapewa na mahakama KSh 1 (shilingi moja) kwa kuwa haki zake zilikiukwa,” jaji Radido alisema.

Mahakama iliamua Omollo alikosewa kwani hakupewa hata sababu yake kutimuliwa kazini.

Upande wa utetezi haukuonyesha kuwa mlalamikaji alipewa sababu hizo na Rais,” uamuzi wa mahakama hiyo ulisema.

Mahakama ilisema wafanyakazi wa umma wanafaa kulindwa chini ya kipengee cha 236 kwenye katiba.

Hata hivyo, jaji Radido alisema Omollo alipatikana na utajiri ambao hakuelezea alipotoa na kwa hivyo shilingi moja inamtosha kama fidia ya kufutwa kazi kwake.

Mahakama awali ilisema Omollo alishindwa kuelezea alipotoa KSh 33M ambazo zilipatikana kwenye akaunti yake.