"> Pigo kwa wafanyakazi wa hoteli licha ya serikali kuahidi kufufua sekta hiyo. – Salaam Fm

Pigo kwa wafanyakazi wa hoteli licha ya serikali kuahidi kufufua sekta hiyo.

Karibu nusu ya wafanyikazi wa hoteli ambao walikuwa wameajiriwa kikamilifu kabla ya janga la Covid-19 kubisha hodi mlango wa Kenya tayari wamerejelea kazi zao  mwishoni mwa Septemba,  ingawa  sekta hiyo bado inakabiliwa na idadi ndogo ya wateja miezi mitatu tangu serikali ilipoanza  hatua za kufungua uchumi.

Utafiti wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) unaonyesha kuwa ni asilimia 44 tu jijini Nairobi na asilimia 10  jijini Mombasa ya wafanyikazi wa hoteli ambao kufikia sasa wamepokelewa kuanza  tena kazi  zao kwa mahoteli mbalimbali baada ya likizo ya lazima ya karibu miezi saba.

Ingawa asilimia 89 ya hoteli nchini zimeanza tena shughuli, kutoka asilimia 35 mwezi Aprili na Mei, sekta hiyo bado inaathiriwa na idadi ndogo ya watalii na wasafiri kando na changamoto kwa wafanyakazi ambao  kwa sasa wengi wamepunguziwa mishahara zao, wengine wakiingia kwa mkataba wa nusu mshahara hadi “hali ya uchumi itakapoimarika”.

Utafiti wa CBK pia uligundua kuwa kwa wastani, asilimia 58 ya hoteli zinatarajia kurejelea shughuli za kawaida (kabla ya Covid-19) katika huduma za malazi na mikahawa mwishoni mwa mwaka ujao, ilhali asilimia 42 hawajui ni lini watafanya hivyo, hali zote zikitegemea  jinsi serikali itakabiliana na janga la COVID-19.

 

“Walakini, hoteli chache zilionyesha kwamba kikwazo kikuu cha kuanza kwa shughuli zao za kawaida ilikuwa gharama kubwa za kufuata itifaki zinazohitajika za kiafya wakati wa mapato ya chini ya biashara.” Ilisoma ripoti hiyo