"> Wateja wa mayai kuchokora mifuko zaidi kupata bidhaa hiyo adimu. – Salaam Fm

Wateja wa mayai kuchokora mifuko zaidi kupata bidhaa hiyo adimu.

Utafiti wa meza yetu ya Uchumi na Biashara imebaini kuwa    wateja  wa mayai nchini   wanalipia zaidi mayai kufuatia uhaba ambao umezidisha gharama  kwa wasambazaji.

Bei za mayai, ambazo zilikuwa zimeshuka hadi Sh280 kwa tray mnamo Aprili, sasa zimepanda  kwa kiasi kikubwa hadi Sh360 kwa tray.

Wamiliki wa maduka jijini Mombasa  wanasema kwa sasa wanalazimika kuuza yai kwa Sh15, au Sh25 kwa mayai mawili, angalau kupata faida.

“Inazidi kuwa ngumu kupata mayai siku hizi kwa sababu ya uhaba katika soko, hali ambayo imetulazimisha kupandisha bei kufidia bei kubwa za jumla,” alisema mmiliki mmoja wa duka.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Ufugaji Kuku Kenya Wairimu Kariuki alisema kupungua kwa usambazaji kunasababishwa na kupunguzwa kwa uagizaji kutoka nje na kupunguza uzalishaji nchini.

 

“Wakati ambapo hatua za kontena ziliwekwa, wakulima walikuwa na ziada na hawakuweza kuiuza mahali popote, wengi wao walilazimika kupunguza juhudi zao za uzalishaji na hii ndio imeathiri usambazaji leo,” Bi Kariuki alisema.

Kenya imekuwa ikipokea mayai zaidi kutoka Uganda na Tanzania  huku wafugaji wa kuku humu nchini wakishutumu hali hiyo kama njia ya kuwanyima soko ya mayai yao na kutaka serikali kuharamisha uagizaji wa mayai kutoka nchi za Uganda na Tanzania.