"> Hatimaye Mwafaka wapatikana kati ya Madaktari na Serikali ya Kaunti ya Mombasa – Salaam Fm

Hatimaye Mwafaka wapatikana kati ya Madaktari na Serikali ya Kaunti ya Mombasa

Hatimaye Serikali ya kaunti ya Mombasa kupitia kwa bodi ya kushughulikia huduma za  umma pamoja na muungano wa madaktari kanda ya pwani wamekubaliana kutimizwa  kwa matakwa ya madaktari baada ya kikao cha pamoja.

Kulingana na mwenyekiti wa bodi  hiyo Farida Abdalla amethibitisha hayo katika kikao kilicho waunganisha pamoja na muungano wa madaktari ukanda wa pwani na kuwataka madatari kutekeleza majukumu yao kama ipasavyo.

Aidha Farida kupitia kwa serikali ya kaunti amewahakikisha wakaazi wa Mombasa  kuwa mikakati kabambe imewekwa na kutekelezwa kuhakikisha kuwa suala kama hilo halitotendeka tena

Haya yanajiri baada ya Madaktari zaidi ya mia mbili kutoa notisi ya kushiriki mgomo katika kaunti ya Mombasa wakilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara yao, kutopata huduma za NHIF sawia na kutopandishwa vyeo.

Hata hivyo kupitia kwa kikao hicho, katibu wa muungano wa madaktari KMPDU kanda ya Pwani Dr. Adiban Mwachi amesema kuwa takriban madaktari 190 wamepadishwa vyeo kama juhudi chanya kwa ushirikiano na serikali ya kaunti .

Vile vile Mwachi ametoa shukrani zake za dhati kwa gavana wa kaunti ya Mombasa Hassana Ali Joho kwa jitihada zake katika sekta ya afya na wafanyikazi wake kwa ujumla .