Kampuni za Mawasiliano nchini mashakani chini ya sheria mpya.

Kampuni za mawasiliano  nchini kama vile Safaricom na  Airtel chini ya sheria mpya ya mawasiliano  ziko kwenye hatari ya kupigwa faini ikiwa zitachukua zaidi ya sekunde 15 kujibu simu za wateja wao wanaotaka usaidizi almaarufu kama Customer Care Services.

Kanuni hiyo mpya iliyochapishwa wiki iliyopita kutoka kwa  maoni ya umma inampa mamlaka ya kudhibiti mawasiliano nchini CAK  kuwatoza faini kampuni za huduma za   mawasiliano     takriban  KSh 300,000 kwa kila ukiukaji  au kifungo   cha hadi miaka mitatu jela.

Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) imeeleza kuwa kupitia kwa sheria hii, wateja wa kampuni za mawasiliano hawataachwa kusubiri zaidi ya sekundi 15 kabla ya kupewa fursa ya kueleza malalamkiko au mapendekezo yao

Kanuni za mawasiliano nchini  zinataka huduma ya wateja wa kampuni hizo kupatikana wakati wote – na utatuzi kwa malalamiko ya wateja kutekelezwa  ndani ya siku 14.

Ikiidhinishwa, kampuni za mawasiliano nchini  zitakabiliwa na faini ya Sh300,000 kulingana na Kifungu cha 27 cha Sheria ya Habari na Mawasiliano ya Kenya 1998 inayowezesha CA kutunga kanuni za huduma za mawasiliano.

Mtu yeyote anayekiuka kanuni yoyote iliyowekwa chini ya kifungu hiki atakuwa ametenda kosa na atawajibika kwa faini isiyozidi Sh 300,000, au kifungo cha muda usiozidi miaka mitatu, au kwa zote mbili,” inasema Sheria hiyo.

Sasa kuna uwezekano kwamba Kanuni hii huenda ikalazimisha kampuni kama Safaricom, Airtel Kenya, Telkom Kenya na Mwananchi Group kuajiri wafanyikazi zaidi kwa vituo vyao vya kupiga simu ili kuwahudumia wateja upesi.

Kufikia sasa, Idadi ya watu wanaotegemea huduma za simu za rununu imeongezeka mara tatu kutoka milioni 19.4 mwanzoni mwa 2010 hadi milioni 55.2 mwishoni mwa Machi 2020.

Kampuni nyingi za simu huwaweka  wateja wanaowapigia simu kusibiri  kwa muda mrefu kabla ya kuwaunganisha na mhudumu, wakati mwingine wakitumia nafasi hiyo  kutangaza bidhaa na huduma zao.