"> Msiepuke huduma za hospitali, wagonjwa wa Malaria wameagizwa. – Salaam Fm

Msiepuke huduma za hospitali, wagonjwa wa Malaria wameagizwa.

Wagonjwa walio na dalili  za ugonjwa wa malaria kama homa na joto mwilini wameagizwa kujiepusha na matibabu mbadala ya kibinafsi kwa uoga wa kutafuta huduma za hospitalini msimu huu wa COVID-19.

Agizo hili  kutoka kwa wizara ya afya linakuja wakati idadi za wanaougua ugonjwa wa COVID-19  wakiongezeka na kufikia 32,803, watu 19055 wakipona na vifo 559 kufikia tarehe 26 Agosti.

Katibu Mkuu  msimamizi katika wizara ya  Afya Dakta  Rashid Aman, 25 Agosti  alisema idadi ya wagonjwa wanaotafuta matibabu kwa ugonjwa wa malaria imepungua kwa theluthi mbili au asilimia 67 kutoka 300,000 hadi 100,000  kwa  kila wiki.

Aman alisema kuwa watu wengine wanaogopa kwamba watapimwa Covid-19 mara watakaporipoti kuwa na homa, ambayo pia ni dalili ya virusi vya korona.

 Wakenya wengi wamejitenga na vituo vya afya kwa sababu wanaogopa kupimwa Covid-19, na ama kulazimishwa kuwekwa kwa karantini na unyanyapaa kutoka kwa jamii,” alisema.

Wengine, alisema, wanadhani wataambukizwa wakati watatembelea vituo vya afya kwa matibabu baada ya Kenya kuripoti zaidi ya 780 za wahudumu wa afya kuugua COVID-19.

“Hizi zote ni dhana potofu kwa sababu wagonjwa wengi wanaoshindwa kutafuta matibabu huishia kuugua malaria sugu usiosikia dawa na ambao unaweza kusababisha athari kubwa  kiafya au hata kuangamia  ikiwa watachelewa kupata matibabu sahihi,” alisema Dk Aman.

Kabla ya janga la korona,Dk Aman amesema mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Malaria ulikuwa ukipima Wakenya milioni tano kila mwaka kwa ugonjwa wa malaria, na kuna uwezekano kwamba serikali haiwezi kufikia lengo hilo mwaka huu kutokana na jitihada zote kuelekezewa maradhi ya  Covid-19.

Kumekuwa na kesi nyingi za wagonjwa kurundika maduka ya kununua dawa kila wanapohisi wagonjwa badala ya kutafuta huduma za madaktari hospitalini, wengine wanaazimia kutumia matubabu ya asili ya majani na kuchemsha mizizi ya miti ilimradi wasiwe na sababu ya kuzuru vituo vya afya ilivyokuwa ada kabla ya ugonjwa wa korona kufika Kenya.