"> Kenya njia panda Somali ikiwekea biashara ya miraa masharti – Salaam Fm

Kenya njia panda Somali ikiwekea biashara ya miraa masharti

Serikali ya Somalia imeipa Kenya masharti matano kabla ya kuondoa marufuku ya uagizaji wa Miraa kutoka Kenya.

Muungano wa  wafanyabiashara wa Miraa  wa Nyambene (Nyamita) unahisi kwamba sharti Kenya itii masharti ya serikali ya Somali ili kuwanusuru wafanyabiashara wa miraa kutoka kwa changamoto wanazopitia kutokana na marufuko hiyo.

Mahitaji hayo ni pamoja na; Kenya lazima iepukane na ubaguzi kwa Somali kidiplomasia, Kenya iepuke  kuingilia maswala ya ndani ya uongozi wa  Somalia, Kenya  kuomba msamaha kwa kukiuka anga ya hewa ya Somalia,Kenya kuruhusu bidhaa kutoka Somali ikiwa ni pamoja na samaki, mchele, sukari, asali, nyama na maziwa kuingia nchini bila masharti na kisha Kenya kuacha kukagua kwa lazima ndege zinazofanya safari kati ya Wajir na Somali.

Mwenyekiti wa Nyamita Kimathi Munjuri ameomba serikali ya Kenya na Somali kuandaa kikao ili kutatua swala hili tata ili kuruhusu usafirishaji wa miraa Somali.

Serikali ya Somali ilipiga marufuku usafirishaji wa vifurushi vya miraa kutoka Kenya mnamo Machi mwaka huu kama njia mmojawapo wa kuthibiti kuenea kwa virusi vya korona chini humo.

Kufikia sasa, serikali ya Kenya haijatoa maelezo wala msimao kuhusu masharti yaliyotolewa na serikali ya Somali.