KEMSA kikaangoni kwa tuhuma za ofisadi.

Ofisi za KEMSA Nairobi

Mweneyekiti wa kamati ya seneti inayoongoza vita dhidi ya corona Sylvia Kasanga, anataka shirika la kusambaza dawa nchini Kemsa, kuwaeleza wakenya waziwazi  kuhusu tetesi za wizi wa vifaa vinavyotumika  dhidi ya mapambano ya corona nchini.

Bi kasanga anasema kuwa wamewaalika maafisa wa KEMSA kufika mbele yao kujibu maswali kuhusu pesa za kununua bidhaa inayosaidia vita dhidi ya korona.

Lazima kila mkenya ajue namna pesa zake kama mlipa ushuru zinatumika, kwa hivyo tumewaalika maafisa wa KEMSA katika kamati ili kutoa ufafanuzi.” Alisema Bi. Kasanga

Aidha kutokana na uzito wa swala hili, Bi Kasanga ametaka bunge la seneti kujiunga na kamati ya COVID-19 kuchunguza swala hili.

Seneta Kasanga anasema maswala mbalimbali yenye uzito katika shirika la KEMSA, yameratibiwa kuchunguzwa kuanzia Leo Jumatatu 10 Agosti.

Kando na KEMSA kueleza swala hili tata , mkaguzi mkuu wa hesabu za  serikali  amepewa makataa ya siku 30 kuwasilisha ripoti kuhusu maswala ya fedha na ununuzi wa vifaa vinavyozingira vita vya korona.

Tunaposubiri kupata majibu kutoka kwa KEMSA, mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali aanze kujiandaa, baada ya siku 30 tutataka atueleze namna ununuzi wa vifaa vya korona ulifanywa, pesa inatumika ila hadi sasa hakuna PPE katika hospitali zetu, aibu” alieleza Bi Kasanga.

Hatua ya kamati ya seneti kuhusu korona inajiri baada ya wakenya kuweka ghadhabu yao wazi kwenye mitandao ya kijamii ambapo Daktari Patrick Amoth ambaye ni kaimu mkurugenzi wa afya aliwajibu wakenya kwamba waelekeze maswali yote yanayofungamana na vifaa vya COVID-19 katika shirika la KEMSA, akisema ndilo lenye uwezo na nafasi bora kujibu kulikoelekezwa vifaa vyenye thamani ya mamilioni ya pesa, misaada kutoka kwa bilionea wa China Jack Maa, miongoni mwa maswala mengine.

Maswala kuhusu uwajibikaji wa pesa za kupambana na COVID-19 unaendelea kuzua tumbo joto miongoni mwa wakenya, huku duru zikiarifu kuwa kuna baadhi ya wakuu serikalini wanaotumia janga la COVID-19 kujinufaisha kupitia shirika moja la kiserikali,hata hivyo afisa mkuu mtendaji wa KEMSA Daktari Manjari Mwangi amepuuzilia mbali dhana hilo.

Awali, magavana wakiongozwa na mwenyekiti wa afya  katika baraza la magavana ambaye pia ni gavana wa Isiolo Mohamed Kuti na mwenzake wa machakos Dakta Alfred Mutua, walitilia shaka uwezo wa KEMSA kusambaza vifaa vya kujikinga dhidi ya virusi vya korona katika ngazi za kaunti.