Viongozi Kilifi wataka serikali za kaunti kusimamia maswala ya aridhi.

Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga akiwahutubia waandishi wa habari mjini Kilifi /Picha na Ericks Mbaruk.

Na Erick Mbaruk

Viongozi wa siasa eneo bunge la Kilifi Kusini wameitaka serikali ya kaunti ya Kilifi kupewa mamlaka ya usimamizi wa masuala ya mashamba.

Kwa mujibu wa mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga mashamba yote yenye vibali vilivyoisha muda wake yanafaa kurejeshwa kwa serikali ya kaunti ya Kilifi.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa eneo la Dindiri, Makata na Kaole, ambao walishirki maandamano makubwa jumanne, wakipinga kufurushwa kutoka makazi yao yaliyo kwenye shamba la takriban ekari 1,700, Chonga amesema tayari amepeleka bungeni mswaada wa kujadili suala hilo.

“Tayari nimepeleka mswaada bungeni kwamba kibali chochote kitakachokuwa kimeisha muda wake hiyo shamba irudishwe kwa serikali ya kaunti. Serikali ya kaunti iko karibu sana na wananchi kuliko ile ya kitaifa na hatutakubali wananchi hawa wafurushwe,” amesema Chonga.

Mbunge huyo ameapa kusimama kidete kuwatetea wakazi wa eneo la Dindiri, Makata na Kaole wapatao 65,000 ambao kwa sasa wanaishi kwa hofu ya kufurushwa katika makazi yao.

Kwa upande wake mwakilishi wadi ya Chasimba Kazungu Mbura ameitaja hatua ya kuwafurusha wananchi kuwa njama fiche kwani bwenyenye huyo hana vibali halali.

“Mradi wowote ambao unaingia katika kaunti ya Kilifi na utakaoishirikisha serikali ya kaunti huwa ni lazima upitie kwa waziri husika wa serikali ya kaunti ,kwa hivyo mradi unaodaiwa kushirikisha serikali ya kaunti na sisi hatujapata taarifa yoyote kutoka kwa waziri basi mradi huo ni wa ulaghai.” amesema Mbura.

Ikumbukwe kuwa endapo wakazi hao watafurushwa basi huenda takriban wanafunzi 3,000 wakaathirika na masomo yao.