Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa azisihi nchi kutoa michango yao

PHOTO: Courtesy

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema umoja huo unakabiliwa na ”mzozo mbaya wa fedha” kwa karibu muongo mmoja sasa,  kwa sababu nchi 64 kati ya 193 hazijalipa michango yao ya kila mwaka.

Guterres, amezitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Marekani, ambayo ndiyo mchangiaji mkubwa wa Umoja wa Mataifa. Nyingine ni Brazil, Iran, Israel, Mexico, Korea Kusini, Saudi Arabia na Uruguay.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema Guterres ameziandikia barua nchi zote wanachama akisema umoja huo uko katika hatari ya kuimaliza akiba yake ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Amesema iwapo fedha hizo hazitatolewa, umoja huo utashindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake. Umoja wa Mataifa umesema hadi jana, nchi 129 zimelipa Dola bilioni 1.9 kama ada zao kwa mwaka 2019. Hata hivyo, Dola bilioni 1.386 bado hazijalipwa kwa mwaka huu.