Maonyesho ya bidhaa mbalimbali za kibiashara kufanyika Dubai

PHOTO: Courtesy

By Noah Mwachiro

Wakenya wamehimizwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kwenye kongamano la 24 la maonyesho ya bidhaa mbalimbali ambalo litafanyika nchini Dubai kwa muda wa miezi sita kuanzia mwezi ujao wa Oktoba hadi mwezi Aprili mwaka ujao.

Akizungumza na wanahabari hapa Mombasa, mwandalizi  mkuu anayesimamia wafanyibiashara wa Kenya nchini Dubai Jalal Balala, amesema kuwa hiyo itakuwa njia moja wapo ya kuonyesha bidhaa mbali mbali za kibiashara ambazo zinatengenezwa nchini kama vile vinyango .

Jalal amesema kwamba nchi ya Dubai huwa iko na amani na kusema kwamba hua inapata watalii zaidi ya milioni saba  kutoka kwa mataifa mbali mbali duniani hivyo basi kuwasihi wakenya kushiriki kwenye maonyesho hayo ambapo bidhaa zao zitapata kuonekana na kununuliwa na watalii hao.

Vile vile amesema nchi zingine 13 za barani Afrika zitakuwa zinashiriki kwenye maonyesho hayo huku akitoa wito kwa serikali kuwasaidia wafanyabiashara wa humu nchini ili kunadi bidhaa zao kwenye kongamano hilo nchini Dubai.