Wahudumu wa afya wagoma Mombasa kufuatia kutolipwa mishahara

PHOTO: Courtesy

By Geoffrey Chiro

Wagonjwa kutoka kaunti ya Mombasa wanaendelea kutaabika baada ya wahudumu wa afya katika hospitali za umma ikiwemo hospitali kuu ya kanda ya Pwani kususia kazi.

Hii ni baada ya wahudumu hao wakiwemo wauguzi, madaktari na maafisa wa afya miongoni mwa wengineo, kufanya mgomo wakilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara yao.

Aidha, wafanyikazi zaidi ya elfu moja wa afya wanaohudumu katika hospitali za umma Mombasa wanashiriki katika mgomo huo.

Peter Maroko, ambaye ni katibu wa wauguzi Mombasa amesema kuwa wafanyikazi hao hawana namna na  mazungumzo waliyoandaa na kaunti yamekosa kuzaa matunda.

Kulingana na Dkt. Chibanzi Mwachonda, ni jambo la kushangaza kuona kuwa katika kaunti zote za Pwani ni Mombasa pekee iliyokosa kulipa mishahara huku kaunti zengine kazi ikiendelea kama kawaida.